|
Bismihi Ta'ala
WITO KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI
"Na
katika haya imekujia HAKI na mauidha na ukumbusho kwa wale wanaoamini." (Suratul
Hud 11:120)
Makala No. 3
MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) ALIMTEUA IMAM ALI (A.S.) KUWA KHALIFA
BAADA YAKE
Katika makala yetu Na.
2, tulianza kutoa ushahidi kutoka katika Qur'an Tukufu na vitabu
vinavyotambulika vya Ahlul Sunnah Wal Jama'ah kuthibitisha kuwa Mtume
Muhammad (s.a.w.w) alimteua Imam Ali bin Abitalib (a.s) kuwa Wasiy na
Khalifa baada yake.
Aidha
katika makala Na. 2, tulitoa uthibitisho wa aina tatu juu ya hilo, na
ushahidi huo ni: (1) Hadithi Indhar au Da'wat Dhul Ashirah. (2) Aya
ya Wilayah. (3) Hadithi ya Manzilah. Katika makala hii Na. 3 na
zitakazofuatia, tutatoa ushahidi zaidi kuthibitisha Uimamu wa Ali bin
Abitalib (a.s).
USHAHIDI Na. 4 - HADITHI YA THAQALAYN : QURAN NA
AHLUL BAYT
Katika Hadithi hii ya Thaqalain, Mtume Muhammad (s.a.w.w) ameripotiwa
akisema:
"INNII TAARIKUN FIIKUM AL-THAQALAYN: KITABULLAHI WA
ITRATII AHLU BAYTII, MAA IN TAMASSAKTUM BIHIMAA LAN TADHILLU BA'DII
ABADAN".
"Ninawaachieni
vitu viwili vizito, kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur'an Tukufu) na kizazi
changu Ahlul Bayt, na ikiwa mtashikamana na hivi vitu viwili, basi kamwe
hamtopotea".
Hadithi hii inathibitisha waziwazi kuwa, kabla ya kufariki, Mtume
alituachia Ahlul Bayt kama viongozi wetu na Imam Ali (a.s) alikuwa ni
kiongozi wa Ahlul Bayt baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), hivyo Imam
Ali ni Khalifa wa Waislamu baada ya Mtume.
Hadithi ya Thaqalayn ambaye imesimuliwa na vitabu vyote vikubwa vya
Ahlul Sunnah Wal Jama'ah na ambayo inachukuliwa kuwa ni hadithi sahihi
kabisa kuliko zote na Maulamaa wote wa Kisunni, peke yake tu ni ushahidi
tosha na ni uthibitisho wenye uzito kabisa unaothibitisha Uimamu wa Ali
bin Abitalib (a.s) baada ya Mtume Muhammad (s).
Imekubaliwa pia na maulama wa Kisunni kuwa hadithi hii imeelezwa na
Mtume, sio mara moja bali katika maeneo na matukio mbalimbali kiasi
kwamba hadithi hii imekuwa maarufu na imesimuliwa na mamia ya
wanahadithi (wapokezi wa hadithi).
Katika moja ya matukio
ambapo Mtume aliitoa hadithi hii ilikuwa ni katika viwanja vya Arafati
wakati wa Hajjatul Widaa' (Hijja ya Mwisho ya Mtume), Siku ya Ghadir
Khum - Mtume alipokuwa anarudi kutoka katika Hajjatul Widaa', katika
siku zake za mwisho za ugonjwa wake, na katika khutba zake katika mji wa
Madina, n.k.
Baadhi ya vitabu
vikubwa vya Kisunni vilivyopokea hadithi hii ni hivi vifuatavyo:
1)
Musnad Ahmad bin
Hambal, Jz. 3, Uk.17
2)
Sahihi Muslim, Juz. 2,
Uk. 237.
3)
Kanzul Ummal, Juz. 7,
Uk. 112.
4)
Sahihi
Tirmidhi, Juz. 2, Uk. 308.
5)
Mustadrak Al-Hakim,
Juz. 3,Uk. 109.
6)
Yanaabi ul
Mawaddah, Uk. 25.
7)
Tafsiir Ibn Kathiir,
Juz. 3, Uk. 486.
8)
Sawa'iq
Al-Muhriqah, Uk. 150.
9)
Taarikh Al-Ya'quubi, Juz.
2, Uk. 93
10) Dhakhair Al-Uqba cha Tabari,
Uk. 16.
Na
vitabu vingenevyo vingi ambavyo hatutavitaja hapa kwa sababu ya uchache
wa nafasi.
Imam Suyuti amesimulia katika kitabu chake: IHYAA'UL MAYYIT,
kwamba katika maradhi ya mwisho ya Mtume (s.a.w.w) Mtume aliwahutubia
sahaba zake kwa kusema: "Enyi watu, ninakaribia kuondoka duniani
kwenda kuonana na Mola wangu Mtukufu, lakini kuweni makini, ninawaachia
vitu viwili: Kitabu cha Allah na kizazi changu Ahlul Bayt". Kisha
aliunyanyua na mkono wa Imam Ali (a.s) na kusema:
"HAADHA
ALI MA'AL QUR'AN, WAL QUR'ANU MA'A ALI, LAA YAFTARIQAANI
HATTAA YARIDAA ALAYYAL HAWDH." - "Huyu Ali yuko pamoja na Qur'an na
Qur'an iko pamoja na Ali, na kamwe hawatoachana mpaka watakaponikuta
katika chemchem (Hawdhi) za Kawthar".
Mtume alituachia Qur'an
na Ahlul Bayt ili tuvishikilie vitu hivi viwili kwa nguvu, ili
tusipotee na tumkute Mtume Peponi katika chemchem za Kawthar kwa
mafanikio. Lakini kwa bahati mbaya baada ya kifo cha Mtume, watu
waliwapuuza Ahlul Bayt na wakaiepuka njia iliyonyooka. Najiuliza nini
litakuwa jibu lao watakapo kutana na Mtume siku ya Hukumu? Mtume ameiita
Qur'an na Ahlul Bayt kama THAQALAYN (Vitu viwili muhimu na
vizito) lakini watu wamevichukulia kiuepesi tu. Tunamuomba Allah
atuepushe kutokanana upotovu na dhulma dhidi ya Ahlul Bayt. Amin.
Na la kushangaza zaidi ni
ukweli kwamba ingawa Hadithi hii ya Thaqalayn ipo katika vitabu vyote
vya Kisunni vinavyo tambuliwa, lakini bado baadhi ya Maulama wa Kisunni
wanajaribu kuuficha kwa sababu wanazozijua wenyewe au ili kuwadanganya
wafuasi wao ambao hawajasoma vya kutosha, kuwa hadithi hii inapatikana
katika vitabu vya Shia tu.
Kuna kipindi niliwahi
kualikwa ili nitoe mada \ hotuba juu ya umuhimu wa elimu katika moja ya
misikiti ya Sunni, Dodoma. Ili kuonyesha elimu walivyokuwa nayo Ahlul
Bayt, niliitoa Hadithi ya Thaqalayn katika hotuba yangu. Baada ya
Majlis (Mkutano), ndugu yetu mmoja Mwislamu Sunni alialikwa kufunga
kikao kwa dua. Yule ndugu yetu alijifanya kuwa ni mwanazuoni mkubwa na
Ahlul Sunnah na badala ya kufunga kikao tu kwa dua' kama alivyotakiwa
kufanya, aliuonyesha wazi ujinga wake \ kutokujua kwake na alionyesha
uadui wake dhidi ya wafuasi wa Ahlul Bayt, kabla ya dua alisema: "Hadithi
ya Thaqalayn, vitu vizito viwili: Quran na Ahlul Bayt haipo kabisa
katika vitabu vya Kisunni na hadithi hii sio sahihi". Uongo gani mkubwa
huu dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake!
Baadaye, baada ya kikao
nilimfuata na kumwambia kuwa nina vitabu vingi vikubwa vya Kisunni kama
Sahihi Muslim, Musnad Ahmad, Riyadhus Swaliheen, n.k. ambamo hadithi
imepokelewa na kuandikwa, na nilimmwalika aje kwangu ili nimpe ushahidi,
lakini hakuthubutu kutokea. Nilitoa vivuli (photocopy) vya kurasa za
vitabu hivi ambamo hadithi imetajwa na nikamtumia, lakini hakujibu wala
hakuonyesha kujuta kwa kitendo chake cha kuikana hadithi ambayo ipo
katika vitabu vyake. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amuongoze katika njia
iliyonyooka - Amin.
AHLUL
BAIT NI AKINA NANI?
Swali
muhimu kabisa ambalo tungependa kulijibu sasa ni Ahlul Bait ni akina
nani? Au Ahlul Bait ni wepi? Hapa pia tutatoa majibu kutoka katika
vitabu vya Sunni tu.
1)
Muslim anasimulia katika Sahihi yake kutoka kwa Safiya bint Shaibah
ambaye aliripoti kuwa: "Siku moja Aisha bint Abubakar alisema: "Siku
moja Mtume wa Allah alikuwa amejifunika KISAA (blanket kubwa), kisha
akaja Imam Hassan (a.s) na Mtume akamuita na kumfunika na Kisaa.
Kisha akaja Imam Husayn (a.s) na pia Mtume
akamfunika. Kisha akaja Fatima (a.s) na Mtume akamfunika kwa Kisaa.
Kisha akaja Imam Ali (a.s) na Mtume pia akamfunika kwa Kisaa. Kisha
akasema:
"INNAMAA YURIIDULLAHU LIYUDH'HIBA ANKUMUR RIJSA AHLAL BAYTI, WA
YUTAHHIRUKUM TATHIIRA". - "Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu
enyi Ahlul Bayt na anataka kukutakaseni utakaso ulio bora kabisa". (Suratul
Ahzab 33:33).
Hadithi
hii inaonyesha waziwazi kuwa Ali, Fatma, Hassan na Hussein
ndio Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ambao wameteuliwa na Mtume
kuwa viongozi wetu. (Angalia Sahih Muslim, Jz.
5, Uk. 287).
2) Katika Sahihi
Muslim imeripotiwa kuwa: "Aya ifuatayo
iliposhuka: "Na atakayebishana nawe baada ya kukujia elimu, mwambie:
Tuwaite watoto wetu na watoto wenu, wanawake wetu na wanawake wenu, na
nafsi zetu na nafsi zenu, na kisha tuombe kwa unyenyekevu laana ya
Mwenyezi Mungu iwashukie waongo (Aya ya Mubahilah, Aali Imran 3:61);
Mtume aliwaiita Ali, Fatima,
Hassan, na Hussein na akasema: "ALLAHUMAA HAA'ULAAI AHLII" -
Ewe Mwenyezi hawa ndio watu wa nyumbani kwangu, Ahlul Bayt". (Tazama
Sahih Muslim, Jz. 5, Uk. 268).
3) Ingawa Mtume
alieleza mara nyingi kuwa Ahlul Bayt ni Ali, Fatima, Hassan, na Hussein;
na hii imerekodiwa katika vitabu vingi vya Kisunni na wapokeaji thabiti,
lakini utakuta baadhi ya wanazuoni wa Kisunni wanajaribu kung'ang'aniza
kuwa Ahlul Bayt ni wake za Mtume.
Ukweli ni kwamba wake za Mtume hawamo katika kundi la Ahlul Bayt, kwa
sababu Ahlul Bayt kwa mujibu wa Qur'an ni Maasumu (hawana madhambi) na
walikuwa wametakasika ambapo wake za Mtume hawakuwa Maasumu. Mjadala juu
ya mada hii utajadiliwa baadaye. Kwa wale wanaoamini kuwa wake za Mtume
ni katika Ahlul Bayt wasome hadithi ifuatayo katika Sahih Muslim,
Juz.5, Uk. 274.
Muslim amesimulia
katika Sahih yake kupitia kwa Zaid bin Arqam ambaye alisema kuwa: "Mtume
Muhammad (s.a.w.w) amesema: "Enyi watu! jueni
kwamba mimi ni mwanaadamu na Malaika wa Mauti anaweza kunijia hata mimi
pia na lazima niitike wito wake. Enyi watu! ninawaachieni vitu vizito
(muhimu) viwili; cha kwanza ni kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambapo ndani
yake mtapata mwongozo na nuru, hivyo shikamaneni na kitabu cha Mwenyezi
Mungu na kamwe msikiache; na kizito cha pili ni Ahlul Bayt wangu,
ninawakumbusheni juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt --- ninawakumbusheni
juu ya wajibu wenu kwa Ahlul Bayt ---- ninawakumbusheni juu ya wajibu
wenu kwa Ahlul Bayt (alirudia mara tatu)".
Kisha tuliuliza:
"Ahlul Bayt ni akina nani, Je wake?" Akasema: "Hapana.
Ninaapa kwa jina la Allah, kwa hakika mwanamke huishi na mumewe kwa muda,
kisha mumewe akimpa talaka, hurudi kwa baba yake na jamii yake, Ahlul
Bayt ni watu wake kutoka katika familia yake na ambao kwao sadaka ni
haramu baada yake". (Sahih Muslim, Baab Fadhail Ali (a.s), Juz. 5, Uk.
274).
4)
Katika Sahih Tirmidhi imeripotiwa kutoka kwa Umru bin Abi Salama ambaye
amesema: "Aya hii iliposhuka: INNAMA YURIDULLAHU LIYUDH HIBA ANKUMUR
RIJSA AHLAL BAYTI WA YUTAHHIRUKUM TAT-HIIRA" - "Kwa hakika, Mwenyezi
Mungu anataka kuwaondeleeni kila aina ya uchafu, enyi Ahlul Bayt, na
kuwatakasani kwa utakaso ulio bora kabisa (33:33)",
katika nyumba ya Ummu Salma, Mke wa Mtume; Mtume aliwaita
Fatima, Hassan, Hussein na Ali na aliwafunika kwa Kisaa (blanketi);
kisha akasema : "Ee Mwenyezi Mungu! hawa ni Ahlul Bayt wangu, hivyo
waondolee kila aina ya uchafu na watwaharishe kwa tohara iliyo bora
kabisa".
Ummu Salma akasema: "Je na mimi ni pamoja nao (Ahlul
Bait) Ewe Mtume wa Allah?" Mtume alijibu: "Hapana, wewe una nafasi yako
na upo katika njia iliyonyooka". Alikataliwa kuingia! Hadithi hii
pia imo katika Musnad Ahmad bin Hambal (Juz 6, Uk. 306), na Sahih
Tirmidhi (Juz. 2, Uk. 209).
5)
Katika aya ya Tathiir: "INNAMAA YURIDULLAHU LIYUDH-HIBA ANKUM
AR-RIJSA AHLAL BAYTI WA YUTAHIRUKUM TATHIIRA (Ahzab 33:33), dhamiri
ya Kiarabu iliyotumika kwa Ahlul Bayt ni "ANKUM......, YUTAHHIRUKUM....".
Wakati katika sura hiyo hiyo katika aya zilizotangulia (Ahzab 33:32-34)
dhamiri iliyotumika kwa wake za Mtume ni "KUNTUNNAA....., MINKUNNA.........,
n.k." ambayo ni dhamiri ya kike kwa kiarabu.
Badiliko hili la ghafla la dhamiri kutoka dhamiri ya
kike kwenda dhamiri ya kiume katika Aya (Ahzab 33:33),
inathibitisha kuwa wake za Mtume hawamo katika Ahlul Bayt ambao
wanatakiwa kufuatwa, kwa sababu wakati Mwenyezi Mungu (s.w.t.)
alipotaka kuwazungumzia wake za Mtume alitumia dhamiri ya kike
"KUNTUNNA ......, MINKUNNA.......", lakini alipoanza kuwazungumzia
Ahlul Bayt "Ali, Fatma, Hassan na Hussein", dhamiri
ilibadilika. Huu ni ushindi dhahiri kwa wale wanaojua sarufi ya lugha ya
Kiarabu.
Wapendwa wasomaji , mmeona kwamba hadithi ya Thaqalayn (vizito
viwili) : Quran na Ahlul Bayt imeripotiwa katika vitabu
vingi sana vya Kisunni, lakini umewahi kumsikia mwanazuoni wa Kissuni
akiizungumzia hadithi hii - Kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt - ambao
ndio ulikuwa wasiyya wa mwisho wa Mtume. Kwanini wanazuoni wa Kisunni
wanaupuuza wosia wa mpendwa kiongozi na Mtume wetu? Je kuna sababu
yoyote ya maana ya kuupuza wosia huu (jambo ambalo ni dhambi kubwa)
zaidi ya kuwa ni ujinga, ugumu wa mioyo, kujiegemeza upande wa imani
zetu ulizonazo, wivu na manufaa yetu binafsi? Tunamuomba Mwenyezi Mungu
atupe tawfiiq ya kushikamana na Qur'an na Ahlul Bayt baada ya Mtume (s.a.w.w).
Amin.
USHAHIDI
Na. 5 - HADITHI YA SAFINA / JAHAZI
Katika
kitabu cha Kisunni : Mustadrak Sahihein imesimuliwa na Hakim kupitia kwa
Hanash Al-Kanani ambaye alisema: Nimemsikia Abudhar Al-Ghafari akisema
wakati alikuwa ameushika mlango wa Ka'ba Tukufu: "Enyi watu, wale
wanaojua mimi ni nani wananijua, lakini wale wasionijua na wajue kuwa
mimi ni Abudhar (Sahaba wa Mtume). Nimemsikia Mtume (s.a.w.w) akisema:
"Mathalu
AHLULBAYTII FIIKUM MATHALI SAFIINATIN NUUH, MAN RAKIBAHA NAJAA, WA MAN
TAKHALLAFA ANHA GHARIKA".
- "Mfano wa Ahlul Bayt wangu ni kama Safina / Jahazi ya Nuuh (a.s).
Kila aliyeipanda aliokoka, na kila aliyejiepusha nayo aligharikishwa".
Mwanachuoni wa Kisunni Hakim amesema kwamba hadithi hii ni Sahihi.
Pia hadithi hii ya Safina imesimuliwa na mamia ya
wanazuoni wa Kisunni katika vitabu vyao. Umewahi kumsikia mwanazuoni
yeyote wa Kisunni akiizungumzia hadithi hii kwenye hotuba yake?
Kama hujawahi , basi wanazuoni hao wanaificha.
Lakini unaweza kurejea vitabu vifuatavyo vya Kisunni na utaipata hadithi
hii:
·
Al-Hakim katika
Mustadrak yake, Juz. 2, Uk.
343.
·
Sawaiq Muhriqah, Uk. 153.
·
Faraid Simtein,
Juz.4,Uk. 149.
· Mustadrak
Sahihein, Juz.3, Uk. 343.
· Nuural
Absaar, Uk. 126;
na vitabu vingine vingi.
Waislamu
waliotaka kunusurika na moto wa Jahanamu siku ya Kiyama waliwafuata
Ahlul Bayt - Imam Ali (a.s), baada ya kuondoka kwa Mtume. Ni sababu gani
inayotufanya tusiwafuate Ahlul Bayt baada ya Mtume na hali ya kuwa Ahlul
Bayt ni safina ya Nuuh (as)?
Kwa
hakika, hatutaki kuwa kama mtoto wa Nuuh (a.s) ambaye juu yake Qur'an
inasema: " ---- na Nuuh alimwita mwanae, na alikuwa peke yake. Ewe
mwanangu! ingia (ndani ya Safina) uwe pamoja nasi na usiwe miongoni mwa
makafiri (wasio amini). Alisema nitakimbilia mlimani, mlima ambao
utanilinda dhidi ya maji. Nuuh akasema hakuna mlinzi leo atakayekulinda
dhidi ya adhabu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule mwenyewe kurehemewa.
Kisha wimbi likapita kati yao, hivyo akawa ni miongoni mwa
waliogharikishwa". (Huud 11:41-43).
Ni nani atakayetuokoa
dhidi ya gharika ikiwa hatutoingia katika jahazi / safina ya Ahlul Bayt?
Tunamuomba Allah (swt) atunusuru na gharika tusiwe kama alivyokuwa
mtoto wa Nuuh. Amin.
USHAHIDI
Na. 6 - HADITHI NYINGINE JUU YA AHLUL BAYT (A.S)
Kuna hadithi nyingi
sana za Mtume Muhammad (saww) zinazoonyesha fadhail na uongozi wa Ahlul
Bayt (a.s). Tutatoa hadithi chache hapa chini kutoka katika vitabu vya
Kisunni ili kuthibitisha nafasi ya Ahlul Bayt baada ya Mtume Muhammad (s.a.w.w):
1) Ibn Abbas
amesimulia kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w) kasema:
"Nyota huwaongoza watu wa dunia ili wasiangamie. Hali
kadhalika Ahlul Bayt wangu ni viongozi wa Ummah wangu watakaouepusha
ummah wangu kutokana na utengano na kutofautiana (kuhitilafiana); na
yeyote miongoni mwa makabila ya kiarabu atakayewapinga, atakuwa ni
kutoka katika kundi la Iblis". (Mustadrak Sahihein, Juz .2, Uk. 343;
Sawaiq Al-Muhriqah, Uk. 235).
Ingekuwa wakureishi
walikubaliana juu ya Uimamu wa Ali bin Abitalib (a.s) na wangekuwa
hawakumpinga Mtume (s.a.w.w) juu ya suala hili, Ummah wa Kiislamu
ungekuwa umeepukana na Utengano na Khitilafu. Lakini kwa bahati mbaya
ukhalifa wa Ali (a.s) ulinyang'anywa, na Ahlul Bayt walipingwa.
2) Jinsi ya
Kumsalia Mtume (s.a.w.w) - Salawat - Mtume Muhammad (s.a.w.w)
amewaelekeza waislamu kuwajumuisha Ahlul Bayt wake (Aali Muhammad)
wakati wa kumtumia salawat, na hairuhusiwi kuiondoa Aali Muhammad kwenye
Salawat.
Kwenye Sahih Bukhari,
imetajwa kwamba siku moja masahaba walimuuliza Mtume Muhammad (s.a.w.w):
"Ewe Mtume wa Allah, tumeelewa jinsi ya
kukusalimia, lakini tufundishe jinsi ya kukutumia salawat (kumsalia
Mtume)". Alijibu: "Semeni
Allahuma swalli
alaa Muhammad wa alaa Aali Muhammad, kama swalayta Alaa Ibrahim wa alaa
Aali Ibrahim, Innaka Hamidun Majid.
(Sahihi Bukhari, Juz.8, Uk. 245).
Swali
hili liliulizwa na masahaba baada ya amri ya salawat kuteremka katika
Qur'an: "INNALLAHA WA MALAAIKATAHU YUSALLUNA ALAN NABII. YAA AYYUHAL
LADHIINA AAMANU SWALLU ALAIHI WA SALLIMU TASLIIMA" - "Kwa hakika
Mwenyezi Mungu na malaika wake wanamtakia rehema Mtume. Enyi
mlioamini! Mtakieni rehema Mtume na msalieni". (Ahzab 33:56).
Maulamaa wa Kisunni na wa Kishia wamekubaliana kuwa aya hii ilishuka kwa
ajili ya fadhail za Mtume na Ahlul bayt wake.
Rejea vitabu vifuatavyo vya Kisunni:
1-
Asbabun Nuzul cha Wahidi,Uk. 271.
2-
Al-Mustadrak cha
Hakim, Juz. 3, Uk. 148.
3-
Tafsiir Fakhruddin
Raazi, Juz. 25, Uk. 226.
4-
Riyadhu Swalihun cha
Nawawi, Uk. 4555
5-
Jami' Li Ahkamil Qur'an cha Qurtubi, Juz.14, Uk. 233-34.
Imesimuliwa
katika Sawaiq Al-Muhriqah cha mwanazuoni wa Kisunni IbnHajar (Uk.
144) kwamba: Mtume Muhammad (saww) alisema: "Msiifupishe
salawat (salawat Al-BATARAA)". Baada
ya kuulizwa nini itakuwa ufupisho wa salawat?
Mtume (s.a.w.w) alijibu: "Mnaposema : Allahuma swalli alaa Muhammad
- na mkaishia hapa, hii haitosihi, lazima mseme: Allahumma
swalli alaa Muhammad wa Aali Muhammad."
Kwa
bahati mbaya ndugu zetu wa Kisunni wanapotuma salawat, wanajiepusha
kusema AALI MUHAMMAD, hivyo wanatoa salawat isiyotimia na wanakhalifu
maelekezo ya Mtume. Kwa mfano katika mawaidha au majlis, wasikilizaji wa
Kisunni, kwa kawaida wanaposikia jina la Mtume humtumia salawat
isiyokamili kwa kusema ALLAHUMMA SWALLI WA SALLIM ALAIHI, bila
kusema WA AALIHI. Hata maulamaa wa Kisunni wanapoandika jina la
Mtume wanaandika salawat isiyotimia SWALLALLAHU ALAIHI WASSALLIM;
wanaondoa "WA AALIHI".
Je ni ujinga au wivu, au kujiegeamiza
upande wao / kujipendelea hata kama sio sahihi au nini, nashangaa?
Katika
hadithi nyingine, Mtume Muhammad (s.a.w.w) alisema: "Yeyote atakaye
sali sala na ndani ya sala yake asinisalie mimi na Ahlulbyt wangu, sala
yake haitokubaliwa". (Tazama : Shifaa ya
Qaadhi Ayadh Maghrabi Juz. 2, Uk. 55; Sawaiq Al-Muhriqa cha Ibn HajarUk.
139).
Mwanachuoni
wa Kisunni Raazi katika Tafsiri yake (Juz.7, Uk. 391) ametaja Ahlubayt
ni sawa na Mtume katika mambo matano: (1) Salawat (2) Salamu
(3) Tahara yaani Ismah (4) Sadaka
kwao ni haramu (5) Kuwapenda ni wajibu.
Imam
Shafii amesema katika shairi lake maarufu kuwasifu Ahlulbayt:
"Ahlulbayt wa Mtume, kuwapenda nyinyi ni wajibu kwa kila
mwislamu kama ilivyofunuliwa kwenye Qur'an. Hii ni fadhail kubwa sana
kiasi kwamba kwa yeyote ambaye hatowatumia salawat, sala yake inakuwa
batili".
3)
Aya ya Mawaddah - "QUL LAA AS'ALUKUM
ALAIHI AJRAN ILLAL MAWADDATA FIL QURBA". - "Sema siwaombi ujira
isipokuwa kuwapenda jamaa zangu wa karibu". (Shura 42:23).
Tafsiri zote na vitabu vya hadithi kwa pamoja vinasema
kuwa Ahlulbayt na Qurba hapa ni Ali, Fatima, Hassan na Hussein, na
kuwapenda ni wajibu kwa kila mwislamu kwa sababu iliposhuka aya hii
Mtume aliulizwa: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni nani hao jamaa
zako wa karibu (Qurba) ambao kuwapenda imekuwa ni wajibu kwa kila
mwislamu? Mtume alijibu: "Ni Ali, Fatima na watoto wao wawili
Hassan na Hussein".
Tazama
: 1.
Sahih Bukhari, Juz. 6, Uk. 129.
2.
Tafsiir Tabara, Juz. 25, Uk. 14.
3.
Tafsiir Al-Kasshaf, Juz. 3, Uk. 402.
4. Tafsiir
Al-Waadhih , Juz. 25, Uk. 19.
Aya hii ya Mawaddah iliposhuka (42:23), baadhi ya watu walianza kuwaza
akilini mwao kuwa Mtume anataka tuwapende Ahlulbayt wake kwa matakwa
yake mwenyewe. Hivyo Jibril alikuja na kumwambia Mtume. Baadhi ya watu
wanakulaumu kwa upendeleo. Hivyo aya hii ikashuka: "Je mnasema
ameitunga Qur'an?" (Shura 42:24).
Alhamdulillah, sisi Shia Ithna Ashariyah tunawapenda Ahlulbayt, na
tunawapa nafasi wanayostahili, tunawafanyia Maulid kila mmoja wao,
tunafurahia furaha zao na hatuzifurahii huzuni zao, na tunaamini kuwa
wao ni viongozi wetu baada ya Mtume (s.a.w.w.). Tunawaita Waislamu wote
kujiunga nasi katika kuwafuata Ahlulbayt baada ya Mtume.
Qur'an inasema katika aya hiyo hiyo ya Mawaddah : "Na yeyote
atakayechuma wema (kwa kuwapenda Ahlulbayt) tutamzidishia wema, kwa
hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani (Shura 42:23).
(Tafsiir Baghawi na Tafsiir Tha'labi). Soma makala Na. 4 kwa
ushahidi zaidi juu ya Ukhalifa wa Imam Ali
bin Abitalib (a.s.).
Wa Billahi Tawfeeq.
Sheikh
Muslim Bhanji
August 2001.
|