|
Bismihi
Ta'ala
WITO KWA WAISLAMU
KUUENDEA UKWELI
"Na
katika haya imekujia HAKI na mauidha na ukumbusho kwa wale wanaoamini." (Suratul
Hud 11:120)
Makala
No. 2
MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) ALIMTEUA IMAM ALI (A.S.) KUWA KHALIFA
BAADA YAKE
Sheikh Muslim Bhanji
Katika
makala yetu Na. 1 tumeonyesha waziwazi
kabisa kuwa Mitume wote waliopita pamoja na mawasii, warithi na
makhalifa wao wote waliteuliwa na Allah (s.w.t) tu, na mamlaka haya ya
kumchagua Mtume au Khalifa hakupewa mtu yeyote katika Ummah.
Kama ilivyokuwa kwa
mitume wote waliotangulia Mtume Muhammad (s.a.w.w) pia kwa amri ya
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimteua Imam Ali bin Abitalib (a.s) kuwa Wasii
na Imam na Khalifa wa Ummah wa Kiislamu baada yake. Alhamdullilah, sisi
Shia Ithna Ashariyah tunatii amri hii ya Allah (s.w.t) kama amri iliyo
juu yetu na tunaamini kwa dhati kuwa Imam Ali bin Abitalib (A.S) ni
Khalifa wa kwanza wa Ummah wa Kiislamu.
Katika hii makala na.
2, tutaonyesha baadhi ya ushahidi kutoka katika Qur'an tukufu, Sunnah na
Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W.W) na kutoka katika Historia ya Uislamu,
ushahidi ambao utathibitisha bila kuacha chembe ya shaka kuwa Mtume
Muhammad (S.A.W.W) hakumteua yeyote isipokuwa Ali bin Abitalib
kuwa wasiy baada yake.
Waislamu wengi na
maulamaa wakubwa wa Ahlul Sunnah Wal Jama'ah baada ya
kuujua ukweli huu walibadili na kuwa wafuasi wa madhehebu ya Kiislamu ya
Shia Ithna Ashariya na sasa wanaamini kwa dhati kabisa kuwa Imam Ali
bin Abitalib ni Khalifa wa kwanza wa Waislamu baada ya Mtume
Muhammad (S.A.W.W). Maelfu ya Waislamu kila mwaka wanaikubali (wanaifuata)
njia ya haki, njia iliyonyooka baada ya kufanya utafiti na baadhi yao
wameandika pia vitabu juu ya utafiti wao. Baadhi ya mifano ya Wanazuoni
wa Kisunni walioingia katika madhehebu ya Shia Ithna Ashariya na
wakaandika vitabu juu ya utafiti wao ni :
a)
Sheikh Muhammad Samawi Tijani wa Tunisia
ambaye baada ya kuwa Shia, aliandika vitabu kama vile: "Hatimaye
Nimeongoka", "Shia ni Wafuasi Halisi wa Sunna ya Mtume", "Waulize
Wale Wanaojua", "Kuwa Pamoja na Wakweli", n.k.
b) Sheikh
Muhammad Mar'iy Al-Amin Al-Antaaqi wa Uturuki ambaye aliandika
kitabu chenye kurasa 520 chenye jina "Kwa nini
nilichagua madhehebu ya Shia - Madhehebu ya Ahlul-Bait (a.s)?"
c) Molwi
Sheikh Hafidh Ali Muhammad Fathuddin Al-Hanafi aliyeandika
kitabu "FULKUN NAJAAT FIL IMAMAH WA-SALAH" (Safina ya wokovu
katika Uimamu na Sala). Kitabu hiki chenye kurasa 328 kinathibitisha
Uimamu wa Ali bin Abitalib na jinsi Mtume (s.a.w.w) alivyokuwa akisali.
d)
Profesa Harun Abdallah wa Nigeria ambaye
ana Shahada ya juu katika Uhandisi wa Madini (Mining engineering),
alifanya utafiti wa kina na aliridhika kuwa madhehebu ya Shia Ithna
Ashariya ni ya kweli. Aliandika kitabu juu ya utafiti wake "The
Missing Link" ambacho kina kurasa 387.
Wapendwa wasomaji,
tuna uhakika kwamba baada ya kusoma makala haya na makala yatakayofuatia,
mkiwa bila upendeleo akilini na ugumu wa kubadilika kutokana na mazoea
na uzoefu wa nyuma, mtaukubali ukweli, na kuamini kuwa wafuasi wa
madhehebu ya Ahlulbait ya Kishia wako katika njia iliyonyooka, wale
ambao Mtume (s.a.w.w) aliwatabiri: "Umma wangu baada yangu
utagawanyika katika makundi 73 na wote watakuwa watu wa motoni isipokuwa
kundi moja". (Al-Mustadrak ya Hakimu, Juzuu 1, Uk. 128; Sunan
Abi Dawood, Juz. 4, Uk. 198; Sunan Ibn
Maajah, Juz. 2, uk. 1321).
Wapendwa wasomaji,
tunawaita katika njia iliyonyooka madhehebu ya Shia Ithna Ashariya,
madhehebu ya Ahlul Bayt (A.S) na jiokoeni kutoka katika moto wa Jahanamu.
Tafadhali jisikie huru kuja kututembelea na kuomba ushahidi na vitabu
zaidi vya rejea. Waislamu walio wengi wanafuata madhehebu ya mashehe wao
na babu zao kibubusa bila kuwa na ushahidi wowote, kama ilivyo kwa wasio
Waislamu wanavyofuata dini za babu zao kibubusa. Qur'an Tukufu
imewalaumu watu wa aina hii ambao hawafanyi utafiti ili kutafuta ukweli:
"Na wanapoambiwa Fuateni aliyoyateremsha
Mwenyezi Mungu, husema: Bali tutafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu.
Je hata kama baba zao
walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?" (Baqara 2:170).
UTHIBITISHO
/ USHAHIDI KWAMBA IMAM ALI (A.S) NI KHALIFA WA KWANZA
Ni ukweli unaoeleweka
wazi duniani kote kwamba kama unataka kumshawishi mtu kuuendea ukweli wa
imani yako, na ikiwa mtu mwenyewe hakubaliani na imani yako, inabidi
utumie mantiki na vitabu vyake yeye mwenyewe anavyovikubali. Kwa mfano
kama unataka kumshawishi Mkristo juu ya Utume wa Nabii Muhammad (s.a.w.w)
inabidi umshawishi kwa kutumia ushahidi ulio katika kitabu chake
anachokiamini : Biblia Takatifu.
Halikadhalika tutatoa
ushahidi kuthibitisha kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimteua Imam Ali (a.s)
kwa amri ya Allah (s.w.t) kuwa wasii wake, kutoka katika Qur'an Tukufu
na vitabu vya Tafsiir, vitabu vya Siirah, vitabu vya Tarikh (Historia),
na vitabu vya Hadithi vilivyoandikwa na Maulamaa wa Kisunni wao wenyewe.
Ushahidi
Na. 1 : Hadithul Indhaar au Da'wat Dhul Ashirah
Katika miaka ya
mwanzo ya kutangaza Uislamu, aya hii iliposhuka: "WA ANDHIR
ASHIIRATAKAL AQRABIIN" - "Na waonye jamaa zako wa
karibu (As-Shu'araa 26:214), Mtume Muhammad (s.a.w.w) alimwita Imam Ali
(a.s.) na akasema: "Ewe Ali, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameniamrisha kuwaita
jamaa (ndugu) zangu wa karibu, hivyo niitie watoto wa Abdulmuttalib
na tuandalie chakula kutokana na nyama ya kondoo na maziwa".
Imam Ali (a.s)
anasimulia kuwa: "Niliwaita kama nilivyoamrishwa na Mtume na
walihudhuria takriban watu 40 ikiwa ni pamoja na ami zake Mtume :
Abutalib, Hamza, Abbas na Abulahab. Walipokusanyika, Mtume
aliwaletea chakula. Ingawa chakula kilikuwa kichache, kiliwatosha kabisa
wote waliokuwepo na bado chakula kingine kikabaki.
Baada ya chakula,
Mtume alipotaka kuzungumza, Abulahab aliingilia kati na kusema: "Huyu
mwenzenu (Muhammad (s.a.w.w) amewaroga", hivyo watu wakasambaa bila
kumsikiliza Mtume. Mtume aliniita tena na kusema:
"Ewe Ali, huyu mtu ameingilia kati na kuzungumza kabla sijazungumza,
hivyo waite tena kesho na utuandalie chakula kama
leo".
Siku ya pili walipokuja,
Mtume (s.a.w.w) aliwaletea chakula na walikula wakashiba kama jana yake.
Walipomaliza kula Mtume alisimama juu na kuwahutubia:
"Enyi wana wa Abdulmuttalib, kwa hakika Mwenyezi Mungu amenituma kwa
watu wote kwa ujumla na kwenu nyinyi niwaite katika Uislamu. Mwenyezi
Mungu ameniamrisha kuwa ni waonye ndugu (jamaa) zangu wa karibu, hivyo
ninawaita katika mambo mawili ambayo ni mepesi
sana katika ulimi lakini ni mazito sana katika mizani (siku ya Kiyama).
Mambo hayo ni Shahada ya Laa Ilaaha Illallah na kwamba mimi ni Mtume wa
Mwenyezi Mungu. Yeyote atakayezingatia (atakayeitikia) wito huu na
kunisaidia atakuwa ndugu yangu, msaidizi (Waziri) wangu, Wasii wangu,
Mrithi wangu na Khalifa baada yangu".
Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi (Ali bin Abitalib) nilisimama na kusema:
"Mimi Ewe Mtume wa Allah". Mtume aliniambia nikae chini na akarudia
tena maneno yale. Hakuna aliyejibu isipokuwa mimi. "Mimi, Ewe Mtume wa
Allah". Mtume aliniambia nikae
chini na akamrudia maneno yale mara ya tatu. Ilipokuwa hakuna
aliyesimama isipokuwa mimi, Mtume aliweka mkono wake katika bega langu
na kutangaza: "HUYU (ALI) NI NDUGU YANGU,
WASII WANGU, WAZIRI (MSAIDIZI) WANGU, WARITHI WANGU NA KHALIFA BAADA
YANGU KWENU, HIVYO MSIKILIZENI NA MTIINI".
Wale
waliohudhuria waliposikia maneno haya, walisimama juu wakicheka na
kumwambia Abutalib: "(Mtume) amekuamrisha umsikilize na umtii mtoto
uliyemzaa mwenyewe!"
Huu ni
ushahidi na uthibitisho wa kwanza katika ushahidi mwingi uliopo, ambapo
Imam Ali bin Abiitalib aliteuliwa kuwa wasiy na Khalifa baada ya Mtume.
Hadithi hii inapatikana katika vitabu vifuatavyo vya Kisunni:
-
Taarikh Tabari - Juz. 3, uk. 560.
-
Sharh Nahjul Balagha cha Ibn Abil Hadiid, Juz. 3, uk. 263.
-
Al-Kaamil cha Ibn Al-Athiir - Uk. 24.
-
Taariikh Jawami cha Suyuti.
- Musnad cha Imam Ahmad bin Hambal;
na vitabu vingine vingi vya Kissuni.
Kwa sababu hadithi hii ni ushahidi uliodhahiri juu ya Uimamu na Ukhalifa
wa Imam Ali bin Abitalib, baadhi ya Maulamaa na waandishi wa vitabu wa
Kisunni, wameanza kujaribu kuificha hadithi hii. Moja ya watu
waliojaribu kuficha hadithi hii ni Muhammad Husayn Haykal wa Misri.
Katika toleo la kwanza la kitabu chake "Hayaat Muhammad" (Maisha
ya Muhammad (s.a.w.w) iliitaja hadithi kwa urefu wake kama ilivyo
Hadithi ya Indhaar, lakini aliiondoa katika toleo lake pili
na la tatu la kitabu hicho hicho kimoja. Kwanini anaamua kuuficha ukweli
na kujipendelea upande wake? Inashangaza. Qur'an tukufu inasema: "Na
msiufiche ukweli kwa uongo na wala msifiche ukweli na hali mnajua". (Baqara
2:42).
USHAHIDI
/ UTHIBITISHO NA. 2 - AYA YA WILAYAH
Ayatul Wilayah ni aya nyingine ya Qur'an inayothibitisha Ukhalifa wa
Ali bin Abitalib (a.s) bila shaka yoyote. Aya hii ipo katika
Suratul Maidah (5:55) ambayo
inasema: "Walii wenu ni Allah, Mtume wake na
waumini wanaosimamisha sala na wanaotoa zakat ili hali ya kwamba
wanarukuu". (5:55).
Maulamaa wote wa
Tafsiir na Hadith, wa Kishia na Kisunni, wanakubali kwamba aya hii
iliteremka kwa ajili ya Imam Ali bin Abitalib (a.s). Baadhi ya
mifano ya wasimuliaji wa hadithi wa Kisunni ni kama ifuatayo:
a) Suyuti amesimulia
katika tafsiir yake katika kitabu chake Tafsiir Durrul Manthur
kwamba Ali bin Abitalib alitoa pete yake kama sadaka
kwa masikini alipokuwa katika sala akirukuu; hivyo Allah akateremsha aya
hii ya Wilayah. (5:55).
b) Mwanazuoni wa
Kisuni Tabrani katika kitabu chake "Awsat" amesimulia kuwa:
"Siku moja maskini mmoja alisimama pembeni ya
Ali ambaye alikuwa katika sala akirukuu (Sunnah) na akaomba chochote,
hivyo Ali akampa pete yake kutoka kidole chake alipokuwa katika Rukuu.
Mtume (s.a.w.w) alipokuja msikitini Imam Ali alimuarifu Mtume juu ya
tukio hili na hapo hapo ikashuka aya ya Wilayah. (5:55).
Mtume alisoma aya hii
kwa sabaha zake na akasema: "MAN KUNTU MAWLAHU
FA ALLIYUN MAWLAHU. ALLAHUMA WAALI MAN WAALAAHU,
WA AADI MAN AADAAHU". Yaani: "Kwa yeyote
ambaye mimi ni kiongozi wake, Ali ni kiongozi wake wa kumtawalia mambo
yake. Ewe Mwenyezi Mungu, kuwa rafiki wa rafiki yake (na Ali)
na kuwa adui wa yule anayeonyesha uadui kwa
Ali".
c) Fakhruddin Raazi
katika Tafsiir yake amesema kuwa Abudhar Al-Ghaffari
alisimulia kuwa: Siku moja Mtume alimuomba Allah kwa kusema : "Ewe
Allah, ndugu yangu Nabii Musa alikuomba kwa kusema kipanue kifua changu,
irahisishe kazi yangu na ondoa uzito katika kauli yangu, ili waelewe
kile ninachokisema na nipatie Wazir (msaidizi) kutoka katika familia
yangu, Haruun ndugu yangu, nizidishie nguvu kupitia kwake na mfanye awe
mshirika wangu katika kazi yangu ----". (Taha 20:25-32).
"Ewe Allah, mimi ni
Muhammad, Mtume wako na mjumbe wako Mpendwa, hivyo ninakuomba ukipanue
kifua changu, uirahisishe kazi yangu na unipe Wazir (msaidizi) kutoka
katika familia yangu, Ali ndugu yangu na niongezee nguvu kupitia kwake
----".
Abudhar anaendelea
kwa kusema : "Wallah, Mtume hakumaliza hata kumaliza dua yake, Jibriil
akaja na kuteremsha aya ya Wilayah (5:55) ambapo Ali alitoa pete yake
kama sadaka kwa masikini alipokuwa akirukuu".
Maulamaa wengine wa
kisunni waliosimulia tukio hili ni : Al-Ganji
Shafii katika Kifayat Al-Talib, Shablanji katika Noorul Absaar, Al-Waahidi
katika Asbaabun Nuzul, Zamakhshari katika Tafsirul Kashshaf, Ibn Hajr
Asqalani katika Al-Kafi Ash-Shafi, Abubakar Ahmed bin Ali Ar-Razi Al-Hanafi
katika Ahkamul Qur'an, Al-Qurtubi Al-Undulusi katika Al-Jami' Li
Ahkamil Qur'an, Shahabuddin Al-Aluusi katika Ruuhul Ma'aani, Sibt ibn
Al-Jawzi katika Tadhkirah, na waandishi wengine wengi wa Kissuni.
Watafiti wa ukweli wanatakiwa warejee vitabu hivyo hapo
juu ili waupate ukweli kuwa Ali bin Abitalib ni Walii, Imam, Khalifa na
Wasii baada ya Mtume kama ilivyo katika aya hii ya Wilaya. (5:55).
Qur'an tukufu
inaendelea katika aya inayofuata kwa kusema: "Na kwa wale
walioukubali Uwalii wa Allah na Mtume wake na wale walioamini (Imam Ali
bin Abitalib), basi kwa hakika kundi la Allah (Shia wa Imam Ali) ndio
wenye kufaulu". (MAIDAH 5:56). Aya hii inafuatia baada tu ya aya
ya Wilaya (5:55).
Kwa bahati mbaya,
baadhi ya watu wanakana Uwalii na Ukhalifa wa Imam Ali bin Abitalib (a.s)
mara tu baada ya Mtume (s.a.w.w). Juu yao Qur'an inasema : "Wanazitambua
neema za Allah, kisha wanazikataa, na wengi wao hawana shukrani". (Nahl
16:83).
USHAHIDI / UTHIBITISHO NA. 3 - HADITH AL-MANZILAH
Wanazuoni wote wa Kishia na Kisunni wanakubali juu ya usahihi wa hadithi
hii. Mtume Muhammad (S.A.W.W) alipokwenda katika vita vya Tabuk katika
mwaka wa 9 Hijria, alimuacha Imam Ali kama
Khalifa wake Madina. Tabuk (katika mpaka wa Syria) ilikuwa ni mbali sana
na Mtume alipaswa kumuacha mtu thabiti na mwenye imani kubwa ili
kuulinda mji mkuu wa Dola ya Kiislamu Madina, kutokana na uovu wa
washirikina, na hususan wanafiki ambao walikuwa wanasubiri wapate nafasi
japo ndogo ili walete mtafaruku Madina. Hivyo Mtume alimteua Imam Ali
ili awe Khalifa wake katika kipindi hiki ambapo Mtume alikuwa safarini.
Wanafiki walianza
kumchokoza Imam Ali kuwa hakwenda Jihad ili kuokoa maisha yake na
kwamba alikuwa anaogopa kifo. Imam Ali hakufurahia maneno haya,
hivyo alikwenda kwa Mtume kumuomba aende naye vitani (Jihad). Mtume
alijibu kuwa haikuwa vizuri kwake yeye Mtume kuondoka bila kumteua Ali
kama Khalifa wake, pale Madina.
Kisha alisema: "AMAA
TARDHAA AN TAKUUNA MINNI BI MANZILATI HAARUNA MIN MUSA, ILLAA ANNAHU
LAA NABIYYA BA'DII" - "Je hauridhiki kwamba wewe kwangu una
nafasi kama ile aliyokuwa Haruni kwa Musa, isipokuwa tu hakuna Mtume
baada yangu?"
Hadithi hii
inathibitisha waziwazi kuwa nafasi ya Ali ni sawa na ile ya Haruni.
Sasa tujiulize ni ipi ilikuwa
nafasi ya Haruni ? Hebu tuiangalie nafasi ya Haruni katika Qur'an Tukufu.
"Na nipatie Waziri kutoka katika familia yangu, Harun ndugu, na
niongezee nguvu kupitia kwake na mfanye awe mshirika katika kazi yangu".
(Taha 20:29-32).
"----- Na Musa alisema kumwambia ndugu yake Haruun; Kuwa Khalifa wangu
miongoni mwa watu wangu ---- ". (A'araf 7:141).
Aya
hizo hapo juu zinathibitisha kuwa Harun alikuwa ni Ndugu, Waziri,
Msaidizi, Khalifa na Mrithi wa Nabii Mussa. Halikadhalika kwa mujibu wa
Hadithi Al-Manzilah, Imam Ali ni Ndugu, Wazir, Msaidizi, Khalifa, na
Mrithi wa Mtume Muhammad baada yake. Je bado tu hamuielewi na
kuitii amri ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) enyi Waislamu!
Hadithi ya Manzilah imesimuliwa na mamia ya Wasimuliaji wa hadithi wa
Kisunni, baadhi yao ni kama ifuatavyo :
-
Sahih Bukhari, Baab Ghazwat Tabuk, Juz. 3, uk. 54.
-
Sahih Bukhari, Baab Manaqib Ali Bin Abitalib, Juz. 2, uk. 185.
- Sahih Muslim, Baab Fazail Ali, Juz. 2,
uk. 236.
- Musnad Ahmad
bin Hambal, Juz. 1, uk. 98 na uk. 236.
- Hakim katika
Al-Mustadrak, Juz. 3, uk.109.
- Suyuti katika
Tarikhul Khulafa, uk. 65.
- Ibn Al-Kathir
katika Usudul Ghaabah, Juz. 4, uk. 26.
- Ibn Hajr Al-Asqalani
katika Isaabah, Juz. 2, uk. 507.
- An-Nisai katika Khasais, Uk. 7 na Uk.
15.
-
Taariikh Ibn Asaakir, Juz. 4, Uk. 96 n.k.
Soma
makala Na. 3 kwa ushahidi zaidi juu ya Ukhalifa wa Imam Ali bin
Abitalib (a.s.). Qur'an Tukufu inasema:
"Na sema: Ukweli sasa umefika (umekuja), na uongo
umeondoka, na daima uongo huwa ni wenye kuondoka".
(Bani Israel 17:81).
Sheikh Muslim Bhanji
July 2001 |