|
Bismihi Ta'ala
WITO
KWA WAISLAMU KUUENDEA UKWELI
- Makala
No. 1
"Na katika haya imekujia HAKI na mauidha na
ukumbusho kwa wale wanaoamini."
(Suratul Hud 11:120)
MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) ALIMTEUA IMAM ALI
(A.S.) KUWA KHALIFA BAADA YAKE
Sheikh Muslim Bhanji
UTANGULIZI
Tofauti kubwa iliyopo baina ya Waislamu wa Kishia na Waislamu wa
Kisunni ni juu ya imani ya Ukhalifa na Uimamu baada ya kuondoka
kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SA.W.W). Sisi waislamu wa Kishia
tunaamini kuwa Imam Ali bin Abi Talib (a.s) ni khalifa na
Imam wa kwanza baada ya Mtume (S.A.W.W) ambapo ndugu zetu
Waislamu wa Kisunni wanaamini kwamba Seyidina Abubakar ( r.a.)
alikuwa ni khalifa wa kwanza.
Ingawa kuna tofauti nyingine ndogo ndogo zilizopo baina ya
madhehebu makubwa ya Uislamu (Shia na Sunni) kwa mfano katika
sheria (Fiqh) kama vile kukunja mikono wakati wa kusali au
kuinyoosha n.k. lakini hizi ni tofauti ndogo ndogo sana ambazo
zinaweza hata kupatikana ndani ya madhehebu manne ya Kisunni (Imam
Shafi, Maliki, Hanafi na Hanbali ). Masuala haya tutayajadili
hapo baadaye InshaAllah.
Mbali na tofauti hiyo kubwa kuna mambo yanayofanana katika
imani za Waislamu wa Shia Ithna Ashariya na Waislamu wa Kisunni.
La
kwanza ni nguzo tano za Uislamu, yaani :
(a)
Shahaada - Laa Ilaaha Illallah - Muhammadur Rasuulullah - Hakuna
mungu apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah - na Muhammad ni
Mtume wa mwisho wa Allah.
(b)
Sala tano za kila siku
(c) Kufunga mwezi wa
Ramadhan
(d) Kuhiji katika nyumba takatifu ya
Kaa'ba
(e) Zakat kwa ajili ya maskini.
Kwa pamoja Shia
Ithna Asheriyya na Sunni wanaamini juu ya kitabu cha mwisho cha
Allah Qur'an kuwa bado kipo vile vile bila mapunguzo au maongezo,
na wanajaribu kufuata maamrisho yake bila kubakiza.
Kwa pamoja Shia
Ithna Asheriya na Sunni wanaichukulia Sunnah na Siira ya Mtume
kuwa ni muongozo kwa Waislamu katika maisha yao ya kila siku na
wanajaribu kuifuata kwa uangalifu mkubwa ili wapate kuokoka hapa
duniani na Akhera.
Ingawa wapo watu
waharibifu katika jamii ambao kwa makosa wanatushutumu sisi Shia
Ithna Asheriya kwa madai mbalimbali ya uongo kama vile kudai
kuwa Shia wana Qur'an yao au madai kuwa eti Shia wanaamini juu ya
Utume wa Imam Ali bin Abitalib, n.k. Wale wote
wanaoutafuta ukweli, wanatakiwa kuyatupilia mbali madai (shutuma)
haya maovu dhidi yetu na tunawaomba watembelee misikiti na
madrassah zetu ambazo mara zote zipo wazi kwa Mwislamu yeyote
kuja kuthibitisha imani zetu.
Kuna Shia zaidi ya
millioni 250 duniani kote ambao wanaamini kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w)
ni Mtume wa mwisho na wanafuata maamrisho ya Qur'an na Sunna za
Mtume (S.A.W.W) katika maisha yao ya kila siku. Katika manispaa
ya Dodoma peke yake, sisi Shia tuna misikiti miwili; Khoja
Shia Masjid na Masjid Imam Mahdi (A.S) na tunawaalika
waumini wote wa Kiislamu kututembelea katika misikiti hii ili
kupata ushahidi kwa macho yao kuhusiana na imani na matendo
yetu kabla ya kuangukia katika mtego wa waharibifu wanaotuzulia
habari za uongo.
KWA NINI SHIA WANAAMINI KUWA
IMAM ALI (A.S) NI KHALIFA WA KWANZA BAADA YA MTUME?
Shia Ithna
Ashariya wanaamini kuwa Imam Ali bin Abitalib ni Khalifa
na Imam wa kwanza baada ya Mtume (S.A.W.W) kwa kuzingatia sababu
moja rahisi sana na iliyo wazi. Sababu hii ni kuwa; "Imam
Ali bin Abitalib (.A.S) aliteuliwa kwa amri ya Mwenyezi Mungu
kuwa Khalifa wa kwanza wa Waislamu na Mtume mwenyewe kwa amri
ya Mwenyezi Mungu (s.wt). Hii ndio sababu na hakuna
sababu nyingine.
Katika Qur'an tukufu (59: 7) Mwenyezi Mungu anasema: "-----Na
anachokupeni Mtume basi pokeeni na anachokukatazeni jiepusheni
nacho".
Qur'an (33:36): "Na haiwi kwa wanamune aliyeamini wala kwa mwanamke
aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri, wawe
na hiari katika shauri lao. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na
Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi"'.
Shia wanaamini kwamba maadamu Mtume (S.A.W.W) mwenyewe kwa amri
ya Mwenyezi Mungu alimteua Imam Ali (a.s) kuwa Khalifa,
Waislamu hawana hiari yoyote isipokuwa kutii amri hii.
MITUME NA
MAIMAMU HUTEULIWA NA
MWENYEZI MUNGU TU NA SI VINGINEVYO
Shia wanaamini kuwa ni Mwenyezi Mungu (Allah) tu ndiye anayeweza
kumteua mrithi wa Mtume na Imam wa Waislamu, na kwamba Ummah wa
Kiislamu hauna hiari yoyote katika jambo hili.
USHAHIDI KUTOKA
KATIKA QUR'AN
Aya za Qur'an zifuatazo zina thibitisha kuwa Mitume wote
na Maimamu waliteuliwa na Allah Mwenyewe.
1)
"Na Mola wako huumba atakavyo na huchagua; Hawana
hiari ya kuchagua" (Qasas 28:68)
2) "Mimi nitaleta
khalifa katika ardhi".
(Baqara 3:30)
3) "Ewe Daud!
Hakika tumekujaalia kuwa khalifa katika ardhi ---- ". (Saad 38
:26)
4) "(Allah)
alisema kwa hakika nitakufanya wewe (Ibrahimu ) kuwa Imam wa
watu (Ibrahimu); alisema Je na katika kizazi changu pia? Akasema (Ndio
lakini) ahadi yangu haitawafikia waovu (madhalimu)". (Baqara 2:124)
5)
"Na tukawajaalia kuwa Maimamu wanaoongoza kwa amri Yetu". (Anbiya
21:73)
6) "Na Unifanyie
Waziri (msaidizi) katika jamaa zangu ........... ndugu yangu Haruni
.......... Mwenyezi Mungu Akasema: Hakika umepewa maombi yako, ewe
Musa". (Taha 20: 29 - 36)
7) "Na hakika
Mwenyezi Mungu alimchagua Adamu na Nuhu na kizazi cha Ibrahimu na kizazi
cha Imrani juu ya walimwengu wote. Ni kizazi cha wao kwa wao;
na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenyekujua". (Ale Imran 3:33 -
34).
8) "Mwenyezi Mungu
amemchagua (Taluti) juu yenu na amemzidishia wasaa wa elimu na
kiwiliwili, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua".
(Baqara 2:247)
9) "Akasema (Allah) : Ewe Musa! Mimi nimekuchagua juu
ya watu wote kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu, basi pokea
haya niliyokupa na uwe miongoni mwa wanao shukuru".
(A'raaf
7:144)
10) "Na tukawafanya miongoni mwao Maimamu
wanaoongoza kwa amri yetu, waliposubiri na walikuwa wakiyakinisha aya
zetu". (Sajdah
32: 24).
Aya zote za Qur'an zilizotajwa hapo juu na nyingine
nyingi ambazo hatukuzitaja zinathibitisha kwamba Mitume wote na
warithi wao waliteuliwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu bila
hiari ya Ummah.
USHAHIDI / UTHIBITISHO WA
KIAKILI NA KIHISTORIA
1) ADA YA MITUME WALIOTANGULIA: Ada ya Mitume wote
ilikuwa ni kuteua warithi wao kwa amri ya Allah bila kuingiliwa na
Ummah. Historia ya Mitume hawa haitoi mfano hata mmoja wa
mrithi wa Mitume aliyechaguliwa kwa kura za wafuasi wake. Hakuna
sababu kwa nini linapokuja suala la mrithi wa Mtume wa Mwisho,
Muhammad (s.a.w.w) sheria na kanuni hii ya Mwenyezi Mungu
ibadilishwe.
Mwenyezi Mungu anasema:
"Wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyezi
Mungu (Mwendo Wake)". (Ahzab 33: 62)
2) MIFANO WA WARITHI WA MITUME
WALIOPITA: Baadhi ya mifano ya warithi wa mitume
walioteuliwa na Mitume waliopita kwa amri ya Mwenyezi Mungu (s.w).
a)
Nabii Adamu alimteua Shiith
b) Nabii Ibrahim alimteua
Ismail
c) Nabii Ya'qub alimteua Yusuf
d) Nabii Musa alimteua Yusho'
bin Nuun
e) Nabii Issa alimteua
Sham'uun
f) Nabii Muhammad ( S.A.W.W)
alimteua Imam Ali Ibn Abi Talib
Qur'an inasema:
"Na wakumbuke waja wetu Ibrahim na Is-haq na Yaqkub
waliokuwa wenye nguvu na busara. Hakika sisi tuliwachagua kwa lile
jambo zuri kabisa la kuikumbuka Akhera. Na bila shaka walikuwa
mbele yetu ni miongoni wa watu bora waliochaguliwa. Na mkumbuke
Ismaili na Alyasaa na Dhulkifli; na hao wote walikwa miongoni mwa watu
bora". (Saad 38:45 - 48).
Qur'an inasema:
"Na hizi ndizo hoja zetu tulizompa Ibrahim juu ya watu
wake. Tunamnyanyua katika vyeo yule tumtakaye. Hakika mola wako ndiye
Mwenye hikima na ndiye ajuaye, Na tukampa (Ibrahim) Is-haq na Ya'quub,
wote tukawaongoa.
Na Nuhu tulimwongoa
zamani. Na katika kizazi chake Daudi na Suleimani na Ayyub na Yusuf na
Musa na Haruni.
Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na tukamwongoza Zakaria na
Yahya na Issa na Ilyasi wote (walikuwa) miongoni mwa watu wema. Na (tukamwongoza)
Ismail na Al-Yasaa (Ilisha) na Yunusi na Luti. Na wote
tukawafadhilisha juu ya walimwengu. Na (tukawaongoa) baadhi ya baba zao
na vizazi vyao na ndugu zao. Na tukawachagua na kuwaongoza katika
njia iliyonyooka. Huu ni uongozi wa Mwenyezi Mungu. Kwa huo humwongoza
amtakaye katika watu wake".
(An-aam 6:83 - 88).
3) MTUME HAKUFARIKI KABLA YA KUMTEUA
MRITHI WAKE (WASII WAKE): Mitume wote waliopita
pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w) hawakupata kuziacha Ummah
zao japo kwa muda mfupi bila kuacha watu watakaoshika mahala pao (warithi).
Hata walipokuwa wanatoka kwa safari fupi walikuwa wanaacha watu
wa kushika mahala pao (warithi). Je inawezekana kwa Mtume
Muhammad (s.a.w.w) kuondoka na kuuacha Ummah wake bila Wasiy (Mrithi).
Mtume Muhammad
alikuwa anajua kuwa muda
wake wa kuondoka duniani umekaribia, alijua kuwepo kwa wanafiki
katika jamii ya waislam, alijua kuwepo kwa watu walioendekeza tamaa ya
madaraka katika mioyo yao, hivyo asingeweza kuuacha Ummah wake bila
wasii (mtu atakayeshika mahala pake). Alimteua Imam Ali bin
Abitalib kwa amri ya Mwenyezi Mungu kuwa mrithi na mtu
atakayeshika mahala pake baada ya kuondoka kwake hapa Duniani.
4) Sababu zinazofanya ulazima wa Mitume
kuteuliwa na Mwenyezi Mungu ni hizo hizo zinazofanya ulazima wa
Wasii, Imamu na Khalifa kuteuliwa na Mwenyezi Mungu kwa
sababu wote wanateuliwa kufanya kazi za Allah.
5) Ikiwa Imam au Khalifa atateuliwa
au kuchaguliwa na watu, utii wake wa kwanza hautakuwa kwa Mwenyezi
Mungu bali kwa watu waliomchagua. Kwa sababu msingi wa mamlaka
yake itakuwa ni watu, mara zote atajaribu kuwaridhisha watu,
vinginevyo ikiwa watapoteza imani juu yake, atapoteza nafasi
yake. Mtu wa aina hii hataweza kutekeleza majukumu ya dini bila
woga au upendeleo, na macho yake daima yatakuwa katika mtazamo
wa kisiasa.
6) Historia ya Uislamu ina mifano tele ya
maovu yaliyofanywa na makhalifa walioteuliwa na wanadamu. Mfano
bora kabisa ni ule wa Yazid bin Muawiya bin Abu Sufiyan
ambaye waziwazi kabisa alizipuuza sheria, alikunywa pombe kweupe,
alimuua mjukuu wa Mtume Imam Husayn (a.s) na alituma jeshi
Makka ambalo liliichoma nyumba tukufu ya Al- ka'aba na kufanya
maovu mengine mengi. (Tazama Taarikhul Khulafaa na Suyuti).
7) Pia ni Mwenyezi Mungu tu ndiye
anayejua hisia na mawazo ya ndani ya wanaadamu, hakuna mwingine
anayeweza kujua undani wa mtu mwingine. Wakati fulani anaweza
kujifanya ni mcha Mungu na mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu ili tu
kuwaonyesha wenzake au ili apate umaarufu ili achaguliwe na wenzake
kuwa kiongozi kwa manufaa ya kiulimwengu.
Mifano ya aina hii
si haba katika historia. Tuchukue mfano wa Khalifa Abdul
Malik bin Marwan ambaye alikuwa anamaliza siku nzima
msikitini akisali na kusoma Qur'an. Siku moja aliarifiwa juu ya
kifo cha baba yake na kwamba watu walikuwa wanamsubiri ili watoe
kiapo cha utii kwake. Aliifunika Qur'an na kusema : "Huku ndio
kuachana kwangu mimi na wewe (Qur'an)". (Yaani kupata Ukhalifa
ndio mwisho wa kusoma Qur'an). (Tazama Taarikhul Khulafaa ya
Suyuti, Ukurasa 217). Sifa muhimu za Imam , ni Mwenyezi Mungu
tu ndiye anayezijua.
8)
MAASUM - Kwa mujibu wa Shia, Maimamu na Makhalifa
lazima wawe Maasum - yaani waliotakasika kutokana na madhambi na
uchafu. Hivyo Maimamu wote 12 walioteuliwa na Mtume Muhammad
(S.A.W.W) walikuwa Maasum (wasio na madhambi), na historia ya Uislamu
inashuhudia umaasumu, ucha Mungu, elimu na tabia njema za Maimamu
12 wa Shia Ithna Ashariyah, wa kwanza wao akiwa Imam Ali bin
Abitalib (a.s.). Mada hii itajadili zaidi katika makala yajayo.
Ismah
(kutakasika kutokana na madhambi ) ni sifa kutoka kwa Mungu
ambayo haiwezi kupatikana kwa jitihada ya mtu tu bila ridhaa ya
Allah, hivyo Maimamu wanatakiwa wateuliwe na Allah tu. Sababu zote
zinazothibitisha kuwa Mitume lazima wawe Maasum pia hizo hizo
zinathibitisha kuwa Maimamu ni Maasum. Maelezo zaidi yatafuatia.
9)
MIUJIZA - Kwa mujibu wa Shia, Maimamu walioteuliwa na
Allah lazima wawe na uwezo kutoka kwa Allah wa kuonyesha
miujiza kila itakapohitajika ili kuthibisha Uimamu wao kama
walivyokuwa wakifanya Mitume. Historia ya Uislamu inathibitisha tena
kuwa Maimamu 12 walioteuliwa na Allah walionyesha miujiza na
waliwashinda maadui zao katika swala la ukweli (haki). Makhalifa
walioteuliwa na watu huwa hawana uwezo wa kuonyesha miujiza, jambo
ambalo ni muhimu sana kwa Mitume na Maimamu.
10)
UBORA - Shia wanaamini kuwa, kama ilivyo
kwa Mtume, Imamu lazima awazidi wale wote anaowaongoza katika sifa
bora kama vile elimu, Ushujaa, Ujasiri, Ucha Mungu, na Ukarimu.
Lazima awe na
elimu kamili ya sheria za Mwenyezi Mungu. Hapa pia, sifa hizi
hazipatikani kwa Khalifa yeyote aliyechaguliwa au kuteuliwa na
watu isipokuwa kwa Maimamu 12 wa Shia Ithna Ashariya walioteuliwa na
Allah. Soma makala atakayofuata kwa maelezo zaidi.
Pointi zote hizi zinathibitisha waziwazi
kuwa warithi, Makhalifa na Maimamu wa Mitume wote lazima
wateuliwe na Allah tu. Maovu yote, kutokuwepo kwa Umoja, Ujinga ,
Uvunjaji wa sheria za kiislamu n.k. yote haya yanatokana na makhalifa
waliochaguliwa na watu waliopinga amri ya Allah kupitia kwa
Mitume wake kuhusiana na suala la ukhalifa.
Ili kupata uokovu, ukweli na utukufu
waislamu wanatakiwa warudi na kufuata amri ya Allah (swt) kuhusiana
na suala la Imam baada ya Mtume, tunawaita katika ukweli na haki.
Lakini ni lini Mtume Muhammad (S.A.W.W) alimteua Imam Ali bin Abi
Talib (a.s) kuwa Khalifa na Imam? Je kuna ushahidi wowote katika
Qur'an tukufu, Sunnah na historia ya Uislamu naothibitisha uteuzi huu?
Ili kupata majibu ya maswali haya soma makala
Na. 2.
June
2001
|